SERIKALI imenunua shamba la Mngeta lenye ukubwa wa hekta 5,818 lililoko Kilombero mkoani Morogoro kutoka kwa mfilisi aliyewekwa na Benki ya NMB baada ya mwekezaji kushindwa kuliendeleza.
Imenunua shamba hilo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha inawekeza katika miradi ya kimkakati, ikiwemo ya sekta ya kilimo na kuleta mafanikio makubwa katika uwekezaji nchini.
Ununuzi wa shamba hilo, umefanyika baada ya serikali kulinunua kwa Mfilisi, Silvanus Mlola aliyewekwa na benki hiyo ambaye ni mdai wa Kampuni ya Kilombero Plantation Limited, baada ya kushindwa kujiendesha na kulipa madeni ya mikopo.
Akizungumza wakati wa kutia saini kwa makabidhiano ya hati na nyaraka mbalimbali za umiliki wa shamba hilo yaliyofanyika katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto, amesema serikali imeamua kununua shamba hilo, kutokana na umuhimu wake kwa Taifa.
Benedicto amesema eneo hilo lina malengo makubwa na serikali kwa kuwa, shamba hilo lipo katika eneo la kimkakati kwa kilimo, litaleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wanaolizunguka eneo hilo.
Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, kampuni hiyo iliwekwa chini ya mfilisi baada ya menejimenti yake kushindwa kuendesha shamba husika kwa faida na kusababisha hasara na madeni makubwa yasiyolipika katika kipindi chote cha makubaliano.
Amesema kuwa, kushindwa kufikia matarajio na makubaliano yaliyofanywa na serikali wakati wa ubia wa kibiashara, ndiyo imefanya shamba hilo kuuzwa na serikali kununua na wana malengo makubwa ikiwemo kuwa na mafanikio makubwa.
“Shamba hili tunakusudia kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili lizalishe mazao ya chakula kwa lengo la kujitosheleza kwa chakula nchini, malengo ambayo hayakufikiwa kama ilivyotarajiwa, hivyo kujiingiza katika mazingira ya serikali kupoteza umiliki wake awali,” amesema.
Na Hamis Shimye





























