CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeagiza ufanyike uchunguzi wa kujitoa kwa mkandarasi wa maji na umeme katika Halmashauri ya Wilaya Geita, kutokana na viashiria vya rushwa na ubadhirifu.
Pia, kimewataka viongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha makusanyo ya sh. bilioni 10 kwa mwaka katika halmashauri hiyo yanasadifu ujenzi wa miradi ya maendeleo na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika Kata ya Mgusu, akiwa kwenye ziara ya wajumbe wa Sekretarieti ya CCM, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na uhai wa Chama mkoani humo.
“Nakuagiza DC (Mkuu wa Wialaya Geita), fanyeni uchunguzi juu ya jambo hili, haiwezekani wakandarasi wajitoe katika miradi bure bure, lazima kuna tatizo hapa.
“Ipo harufu ya rushwa hapa, fanyeni uchunguzi kubaini ni nini kinasababisha wakandari hawa kujitoa. Tusije tukawalaumu kumbe tatizo lipo kwetu,” alisema Shaka wakati akikagua Ujenzi wa Zahanati ya Mgusu.
MAKUSANYO YASADIFU MAENDELEO
Akizungumzia makusanyo ya halmashauri hiyo, alisema amepewa taarifa kuwa, kwa mwaka inakusanya zaidi ya Tsh.bilioni 10, lakini fedha hizo hazilingani na miundombinu na huduma za maendeleo zinazotekelezwa.
“Hapa napo huenda kuna dalili za ubadhirifu, hili lazima tulitazame kwa karibu na kulifanyia kazi. Makusanyo haya ni makubwa, haiwezekani tusione kasi ya maendeleo wilayani hata barabara hazina taa,” alisema.
Alisema wananchi wanalalamika kwamba ingawa kuna tarakimu nzuri za makusanyo, lakini uzuri wake hauonekani katika uboreshaji wa mji huo na huduma za kijamii.
“Wananchi wanalalamika kutokuwepo kwa miundombinu na huduma bora, mfano; barabara nyingi hazina taa, zahanati za vijiji vingi zimekamilika muda mrefu lakini, hazijaanza kutoa huduma, masoko ya wafanyabiashara wadogo kukosa mazingira rafiki ya kufanyia biashara kwa kisingizio cha ufinyu bajeti. Hii haiko sawa,” alisema.
Shaka aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha Makusanyo ya mapato yanaendana na miradi ya maendeleo.
MBUNGE
Awali, akizungumza mbele ya Shaka, Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu, alisema kazi kubwa inafanyika katika jimbo hilo lililopo wilayani Geita na kufanikiwa kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi.
Hata hivyo, alisema zipo baadhi ya changamoto zinazolikabili jimbo hilo, ikiwemo ya baadhi ya vijiji kutofikiwa na umeme, baadhi kutoka kata ya Mgusu na kuongeza kwamba, changamoto nyingine ni ya majisafi na salama katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.
WALICHOSEMA WATAALAMU
Akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa katika kikao hicho, Mhandisi wa Umeme wa Mkoa wa Geita, Gosbert Gowele, alisema tayari fedha zimeshatolewa kwa ajili ya kukamilisha usambazaji umeme katika vijiji vyote vya mkoa huo.
Akizungumzia mradi wa REA ambao ungefikisha umeme katika Kata ya Mgusu, alisema mkandarasi aliyepitishwa kutekeleza mradi huo alijitoa na mchakato wa kumpata mwingine unaendelea.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Maji, Baraka Mohammed, alisema wanaendelea kusimamia upatikanaji wa huduma hiyo na kuongeza, mkandarasi aliyepitishwa kutekeleza miradi ya maji Geita aliondolewa.
MAAGIZO MENGINE YA SHAKA
Mbali na hayo, Shaka alitaka kuwepo uwazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuitenganisha inayogharamiwa kwa mapato ya ndani, ruzuku ya serikali kuu , ili kuleta tija kwa wananchi na kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kwa ufanisi.
Pia, aliagiza wachimbaji wadogo zaidi ya 2,000 katika Kata ya Mgusu wasikilizwe ombi lao la kuongezewa eneo kutoka msitu wa Geita, ili wafanye shughuli zao kwa amani na utulivu.
Na MWANDISHI WETU, Geita




























