EMMANUEL MOHAMMED NA HANIFA RAMADHANI, ZANZIBAR
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Rais mstaafu wa Zanzibar, ameeleza kuridhishwa na kasi ya utendaji ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Dk. Shein amemuomba Rais Mwinyi aendelee kuchapa kazi na kuhakikisha anatekeleza kwa ufanisi ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.
Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akiongoza kikao maalumu cha siku moja cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar, kilichofanyika Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na wajumbe wa Kamati Maalumu ya NEC CCM, Taifa Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine kilipokea na kujadili taarifa ya wana CCM wanaomba kugombea nafasi ya Ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Aidha, kikao hicho kilipokea na kujadili taarifa ya ziara ya Rais Dk. Mwinyi aliyoifanya mikoa sita ya CCM Kichama.
Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Shein alieleza kuridhishwa na kasi ya utendaji ya Rais Dk. Mwinyi na kumuomba aendelee kuchapa kazi na kuhakikisha anatekeleza kwa ufanisi ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.
Dk. Shein aliwataka wajumbe kuendelea kufanya kazi za Chama Cha Mapinduzi kwa bidii ili kuhakikisha Chama kinaimarika zaidi.
Kwa upande wake, Rais Dk. Mwinyi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, alisema kazi kubwa iliyopo mbele yake ni kuhakikisha mambo mengi yaliyoainishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 yanatekelezwa kwa wakati muafaka.
Alisema bajeti hiyo imebeba mahitaji muhimu ya makundi yote katika jamii, hivyo wananchi watarajie kupata huduma bora za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.
Pia, alisema serikali inajipanga kuanza ujenzi wa barabara za ndani zenye urefu wa kilomita 220 na barabara kuu kwa urefu wa kilomita 200 kwa Unguja na Pemba ili kuwarahisishia wananchi huduma za usafiri.
“Tumejipanga vizuri kutatua changamoto za upungufu wa maji, kujenga na kukarabati barabara za ndani na kuu na kuimarisha huduma za afya,” alisema.





























