WAZANZIBARI wametakiwa kuyalinda maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa, ambayo yamejenga umoja na mshikamano.
Wameelezwa huo ndiyo urithi ulioachwa na Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye hadi anakutwa na mauti alikuwa katika juhudi za kuhakikisha umoja unaimarika kwa maslahi ya watu wote.
Hayo yamesemwa visiwani hapa na Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.
Sherehe hizo zilikwenda sambamba na kuzinduliwa kwa taasisi ya Foundation ya Maalim Seif katika hoteli ya Golden Tulip, Unguja.
Amesema Hayati Maalim Seif ameacha mfano mzuri katika muda wa maisha yake, ameutumia kwa ajili ya kujenga umoja na mshikamano katika sehemu zenye mifarakano, baada ya watu kutofautiana kwa misimamo mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
”Tuyalinde maridhiano ya kisiasa kwa faida ya kizazi kijacho ambapo hapa tunajifunza tunapopingana kwa hoja vikao vinaleta suluhu,” alisema Samia.
Amesema kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yapo mambo mengi ya kujifunza kwa sababu Maalim Seif, ametumia muda mwingi wa ujana wake akiwa katika CCM na kushika nafasi mbalimbali za uongozi hadi kuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
Amesema Chama kitamuenzi na kumkumbuka Maalim Seif kwa sababu ameacha alama nzuri katika harakati za uongozi inayohitaji kuigwa na viongozi wengine wanaochipukia hususan vijana.
Kwa mfano katika kipindi chake atakumbukwa alikuwa baba wa demokrasia ya mageuzi ya kiuchumi na ndipo alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa Rais wa Zanzibar.
”Uwezo na sifa za uongozi ndiyo zilizomsukuma aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi kumteua Maalim Seif kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akiwa baba wa mageuzi ya demokrasia kuelekea katika mfumo wa vyama vingi katika mwaka 1989-1992,” alisema.
Awali, Rais Samia aliwataka wanasiasa kuwa tayari kutafuta maridhiano ya kisiasa sehemu zenye mifarakano na chuki kwa ajili ya kuwaunganisha wananchi na kuondosha tofauti za kisiasa.
Alisema wanasiasa hawatakiwi kukata tamaa hata pale mambo wanapoona yanaharibika na kwenda kombo kama ilivyowahi kujitokezaa kwa Maalim Seif kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akitafuta suluhu ya kudumu.
Alisema Maalim Seif angekuwa mtu wa kukata tamaa maridhiano yaliyopo kamwe yasingefikiwa na leo hii tungekuwa tunazungumza mifarakano na mivutano ya kisiasa kila siku.
Rais Samia alisema kwa nyakati tofauti juhudi za kuleta maridhiano ya kisiasa zilianzishwa, lakini ziligonga mwamba kwa sababu mbalimbali ikiwemo mwafaka wa kwanza hadi wa pili na baadaye kuazaa matunda kwa mwafaka wa tatu mwaka 2010 chini ya juhudi kubwa za Rais Mstaafu Amani Abeid Karume.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar, Dk.Hussein Ali Mwinyi alisema pengo la Maalim Seif haliwezi kuzibika kwa sababu alifanya kazi kwa kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kuona watu wanaishi kwa amani na utulivu.
”Tuishi duniani kwa kuiga tabia za Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa si mtu wa kujikweza wala kujenga kiburi kwa wengine…alikuwa tayari kuwasaidia watu na nchi yake kuona mafanikio yanafikiwa,”alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema madhumuni ya kuanzishwa taasisi ya Maalim Seif ni kuendeleza kazi na juhudi na fikra sahihi zilizoanzishwa na kiongozi huyo.
Alisema Chama cha ACT-Wazalendo kimeingia katika maridhiano ya kisiasa kwa ajili ya kuimarisha amani na kuona Zanzibar inapiga hatua kubwa ya maendeleo, ambapo amewahakikishai wananchi, Rais Samia na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi watalinda maridhiano kwa nguvu zote.
Na MWANDISHI WETU, ZANZIBAR





























