WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema silaha 228 zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria, zimesalimishwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini, huku ikionekana tatizo la utengenezaji wa silaha za kienyeji, yakiwemo magobore ni kubwa nchini.
Amezitaja silaha hizo kuwa ni bastola tano, magobore 174, shortgun 38, rifle 10 na SMG, ambazo ni sawa na asilimia nne ya silaha zote zilizosalimishwa.
Pia, amesema ipo mitutu 12 iliyosalimishwa ambayo kati ya hiyo, 11 ilisalimishwa Mkoa wa Tanga na mmoja Mkoa wa Mbeya.
Simbachawene alitangaza hayo jijini hapa alipokuwa akizungumzia kuhusu tangazo la msamaha wa usalimishwaji wa silaha zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria.
Alifafanua kuwa kati ya silaha zilizosalimishwa imeonekana magobore ni asilimia 76.3.
“Jambo hilo linaonyesha kuwa tatizo la utengenezaji wa silaha za kienyeji, yakiwemo magobore ni kubwa hapa nchini,” alieleza.
Simbachawene alisema baada ya tangazo la msamaha huo kukamilika, ameliagiza Jeshi la Polisi kufanya misako kwa kutumia taarifa za kiintelejensia kuwabaini na kuwakamata wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na kuwachukulia hatua za kisheria.
Aidha, aliliagiza kuangalia upya uwezekano wa kufanya marekebisho ya sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha na risasi ya mwaka 2015, ili kuweka utaratibu wa kisheria wa kutengeneza na kuruhusu magobore kwa kuwa silaha hizo zimekuwa zikitumika kwa shughuli za ulinzi katika jamii, lakini pia watu wasio na nia njema hutumia kufanya uhalifu.
“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi zitakazosaidia kuwabaini wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria ili sheria ichukue mkondo wake,” alisisitiza.
Oktoba 30, mwaka huu, waziri huyo alitangaza msamaha wa kutoshitakiwa kwa yeyote atakayesalimisha silaha kwa hiari kuanzia Novemba mosi hadi 30, mwaka huu.
Waziri huyo alichukua uamuzi huo kwa mujibu wa tangazo la Serikali Na. 774 la Oktoba 29, mwaka huu, ambalo liliainisha masharti ya usalimishaji wa silaha kwa hiari.
Hatua hiyo ya kutangaza msamaha kwa watakaosalimisha silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria, ilitokana na mamlaka aliyonayo waziri wa mambo ya ndani ya nchi, chini ya kifungu cha 64 cha sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha na risasi ya mwaka 2015.
Na Benedict Mwasapi, Dodoma





























