NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameagiza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam, kuhakikisha maboresho yanayofanywa katika ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), yanakamilika ifikapo Juni, mwaka huu.
Agizo hilo alilitoa, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo na kuwataka wataalamu wanaosimamia maboresho ya barabara hiyo, waendelee na utoaji elimu kwa madereva na watumiaji wengine ili kupunguza ajali.
“TANROADS shirikianeni na askari wa usalama barabarani kutoa elimu ya namna bora ya kutumia vivuko vya juu na chini ya barabara, pindi ujenzi wake unapokamilika na kuhakikisha barabara zinakuwa safi wakati wote,” alisisitiza.
Amewaonya wote wanaoharibu alama za barabara na kutupa taka ngumu, kuacha mara moja uharibifu huo na kuwataka wasimamizi wa barabara kuwachukulia hatua za kisheria mara moja.
Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Harun Senkuku alimhakikishia Kasekenya kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), yenye urefu wa kilomita 19.2, uliohusisha madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji umekamilika na sasa ni uboreshaji wa njia ya mwendokasi.

Amezitaja kazi nyingine zinazoendelea ni ujenzi wa madaraja mawili ya juu eneo la Mbezi Mwisho na Kwa Yusuf ili kupunguza msongamano katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani cha Magufuli.
Kazi nyingine ni kujenga barabara ya maingilio katika kituo hicho, kujenga kituo cha mabasi ya daladala eneo la Kibamba njia ya Mloganzila na kuongeza taa za kuongozea magari eneo la makutano ya barabara ili kurahisisha uvukaji wa magari na watembea kwa miguu.
Sh. bilioni 218, zinatarajiwa kutumika katika mradi huo hadi utakapokamilika Juni, mwaka huu.
NA MWANDISHI WETU



























