KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma imetembelea na kukagua ujenzi wa Vyumba vya Madarasa yanayojengwa kwa kutumia fedha za Uviko-19 huku ikipongeza uongozi wa jiji la Dodoma chini ya Mkurugenzi wake Joseph Mafuru kwa utekelezaji thabiti wa miradi hiyo ambao umefikia asilimia 90.
Pia imeliagiza jiji hilo kuhakikisha ujenzi huo kendana na utuunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa lengo la kutnza mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma baada ya kumalizika kwa ziara hiyo ambapo wamekagua vyumba vya madarasa katika Shule za Sekondari za Miyuji, Umonga, Kiwanja cha ndege, Viwandani, Itega na Dodoma Sekondari ikiwa ni pamoja na kukagua karakana zinazotengeneza Madawati.
Mtaka ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma ameonyesha kuridhishwa na Ujenzi wa Madarasa hayo huku akisema ni vyema Ujenzi wa Vyumba hivyo vya Madarasa ukazingatia suala zima la upandaji miti katika utunzaji wa Mazingira.
“Sasa nipende kuwaagiza kuwa lazima Ujenzi huu uendane na thamani ya pesa kama Mheshimiwa Rais ambavyo amekuwa akisistiza Kila siku lengo hapa ni kuona watoto wetu wananufaika na miradi hii.”amesema
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wazazi na walenzi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuhakikisha ifikapo Januari 17 Mwaka 2022 watoto wote wawepo shuleni.
“Kwanza ni wapongeze sana kwa hatua hii ni hatua kubwa na inayoleta matumaini naisistiza kwa jinsi Mradi wa ujenzi wa Vyumba hivi vya Madarasa unavyoendelea mmenihakikishia mmefikia asilimia 90 ya Ujenzi nataka tarehe hiyo 17 Januari watoto wote waripoti Shuleni ili wapate haki yao ya msingi kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla,”amesisitiza.
Pia, ameutaka uongozi wa jiji hilo kuhakikisha wanakamilisha Ujenzi huo wa vyumba vya Madarasa kwa wakati ili watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa masomo waweze kusoma.
Naye Katibu Tawala mkoa wa Dodoma, Fatma Mganga amesema Dodoma ilikuwa na upungufu wa madarasa ya sekondari 601 huku Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akisema wanatarajia kupokea wanafunzi 10,755 kidato cha kwanza 2022 Mwaka huu watakabidhi Madarasa hayo.
Awali Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Joseph Mafuru ameihakikishia Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dodoma kuwa hadi ifikapo Disemba 24 Mwaka huu watakabidhi Madarasa hayo.
“Sisi kama Jiji tunajitahidi katika kutekeleza Mradi huuu na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kuona umuhimu wa watoto ambao walikuwa wanakosa nafasi kuweza kusoma,”amesema.
Amesema mafanikio ya kiwango hicho cha utekelezaji wa mradi kwa asilimia 90 kimefikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa baina ya uongozi na watendaji wa jiji ambao ndio watekelezaji na wanaamini pasina shaka asilimia 10 iliyobaki itakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Fredrick Mwakisambwe akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa 147 yanayotekelezwa kupitia Mradi huo wa Uviko-19 katika Halmashauri hiyo amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya juhudi kubwa ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Miradi hii inafanyika kwa kuzingatia kiwango cha ubora yani thamani ya Fedha ambapo ujenzi huo unaenda sambamba na utengenezaji wa Madawati,” amesema
Na Happiness Mtweve Dodoma





























