WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, ametoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusu kusitishwa kwa kutua kwa ndege za Shirika la Emirates na Flydubai, katika Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), kutokana na kutokuridhika na huduma za upimaji wa Corona ambapo amesema timu ya watalamu wanafanyia kazi tatizo hilo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uwnaja huo wa ndege baada ya kupokea chanjo aina ya Sinopham, Waziri Ummy ameahidi mashirika hayo kuwa, serikali itatatua changamoto hiyo haraka iwezekavyo, ambapo ametoa siku saba kwa timu ya watalamu wa wizara kukaa pamoja na kukamilisha huduma zinazokidhi mahitaji.
“Niahidi mashirika hayo ya ndege ya Emirates na Flydubai kuwa jambo hili kwetu ni muhimu sana kwa sababu za kiuslama na kiuchumi, hivyo wataalamu wafanye haraka iwezekanavyo nimeshaanza mazungumzo na wizara ya uchukuzi kwa kumshirikisha Waziri Mbalawa, ili kuanza huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wetu,”amesema.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema ushirikiano baina ya nchi yake na Tanzania katika mapambano ya ugonjwa huo ni muhimu.
Amesema msaada huo wa chanjo 800,000 kutoka nchini China ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa nchi hiyo kusaidia Afrika, katika mapambano ya pamoja ya ugonjwa huo unaosumbua dunia.
NA MARIAM MZIWANDA





























