SERIKALI imesema idadi ya watalii wanaoingia nchini imeendelea kuongezeka hadi kufikia watalii milioni moja na nusu ikiwa ni matokeo ya mkakati wa kutangaza vivutio vya utalii kimataifa.
Akizungumza jijini Dodoma kuhusu mafaniko ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mary Masanja, alisema kwamba, ongezeko hilo limewezesha taifa kuingiza pato lenye thamani ya dola bilioni 2.6.
Alisema katika kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi, serikali imeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa na kushiriki makongamano, maonyesho na ziara za utangazaji utalii.
Alitaja masoko hayo kuwa ni Uingereza, Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Hispania na Australia huku masoko ya mkakati yakiwa ni China, Urusi, India, Poland, Jamhuri ya Czech, Israeli, Uturuki, Falme za Kiarabu, Qatar, Kuwait na Saudi Arabia.
“Katika miaka 60 iliyopita, serikali iliimarisha utalii nchini kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mikakati ya kukuza vivutio mbalimbali vya utalii vikiwemo hifadhi za wanyamapori, maporomoko ya maji, milima, misitu ya mazingira asilia, utamaduni, fukwe na malikale.
Aliongeza kuwa: “Kupitia uendelezaji wa vivutio hivyo, Tanzania imeweza kupata mafanikio mbalimbali yakiwemo kuongezeka kwa idadi ya watalii na mapato.”
Alifafanua zaidi kwamba, kutokana na juhudi hizo, idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka nchi mbalimbali, imeongezeka kutoka 9,847 mwaka 1960 hadi kufikia watalii 1,527,230 mwaka 2019.
Kadhalika, alisema kumekuwa na ongezeko la mapato yatokanayo na watalii kwa mwaka 1995, yalikuwa dola milioni 259.44, yaliendelea kuongezeka hadi kufikia dola bilioni 2.6 mwaka juzi kabla ya ugonjwa wa UVIKO-19.
“Kutokana na jitihada za Serikali katika kukabliliana na ugonjwa wa UVIKO-19, idadi ya watalii imeanza kuongezeka kutoka watalii 620,867 mwaka jana hadi kufikia 716,169 Oktoba, mwaka huu,” alisema.
AJIRA SEKTA YA UTALII
Naibu waziri huyo, alieleza kuwa wananchi wameendelea kushiriki shughuli za utalii ambapo ajira milioni 1.6 za moja kwa moja na zile ambazo si za moja kwa moja, zimepatikana.
“Katika kuendelea kujenga mazingira bora ya kuwawezesha wananchi hususan vijana kuanzisha biashara za utalii nchini, serikali imepunguza viwango vya ada ya leseni kutoka wastani wa sh. milioni tatu hadi sh. milioni moja.
“Hatua hii imelenga kuongeza ushiriki wa wakala wa biashara za utalii ambao ni wazawa katika biashara za utalii. “Kufuatia hatua hiyo, wakala wa biashara za utalii, wazawa waliongezeka kutoka wakala 643 hadi kufikia 1,687 sawa na ongezeko la asilimia 162.4,” alibainisha.
Kuhusu vivutio vya utalii, alisema vimepata umaarufu mkubwa na tuzo mbalimbali za kimataifa.
Alieleza kuwa, Hifadhi ya Taifa Serengeti imekuwa bora zaidi barani Afrika katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka juzi hadi mwaka huu.
Pia, alisema hifadhi hiyo imetambuliwa na jarida maarufu la Forbes la Marekani kama kivutio cha pili duniani miongoni mwa vivutio bora 21 vya kutembelewa kwa mwaka 2021.
Aidha, alibainisha kuwa Hifadhi za Taifa za Kilimanjaro, Serengeti na Tarangire, zimeshinda tuzo ya kuwa hifadhi bora kati ya 20 za kwanza duniani mwaka huu.
“Pamoja na mafanikio hayo, Tanzania kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), imetangazwa kuwa mshindi wa kundi la dhahabu miongoni mwa washindi 51 kutoka nchi 39 duniani wa tuzo ya huduma za viwango vya kimataifa kwa mwaka jana.
“Pia hifadhi tano za taifa ambazo ni Kilimanjaro, Serengeti, Mkomazi, Manyara na Arusha, zimepata tuzo ya ubora wa huduma za viwango vya Kimataifa kwa mwaka 2020,” alieleza Naibu waziri huyo.
Na FRED ALFRED, Dodoma



























