MPANGO Kabambe wa Kupeleka Nishati Vijijini, umelenga kuwanufaisha wananchi kupitia usambazaji umeme na nishati bora ya kupikia.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki mkoani Kigoma wakati wa ziara ya viongozi wakuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, walisema mpango huo unahusisha nishati za aina mbalimbali, siyo umeme peke yake.
Wakili Kalolo alisema ni jukumu la REA kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanapata nishati safi na zenye gharama nafuu ili ziwasaidie kuboresha maisha yao, hivyo umejiwekea mikakati ya kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa ipasavyo.
“REA imefanikiwa kwa kiwango kikubwa na inaendelea kufanya vema katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hivyo hakuna shaka katika utekelezaji wa miradi ya aina nyingine za nishati zilizofanyiwa tafiti, utakuwa wenye ufanisi,” alisema.
Akitoa mfano, alisema kuwa tafiti zinaonesha eneo lingine muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ni katika nishati ya kupikia ambapo asilimia kubwa ya waathirika ni wanawake, ambao kutokana na matumizi ya kuni, wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya macho na kifua.
Alisema ni kwa sababu hiyo, Wakala umedhamiria kuondoa adha hiyo katika jamii hususani wanawake waishio vijijini.
Mkurugenzi Mkuu REA, Mhandisi Saidy, akiuelezea zaidi mpango huo, alisema umejikita katika sehemu mbili kubwa ambazo ni usambazaji umeme na nishati ya kupikia.
Alieleza zaidi kuwa, hivi sasa REA inaongeza nguvu katika nishati ya kupikia ili kuhakikisha wananchi hususan wa vijijini, wanatumia nishati bora kwa shughuli za kupikia na kupunguza au kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa, ambao upatikanaji wake ni mgumu, ghali na sio rafiki kwa mazingira.
Mhandisi Saidy alisema REA imefanya utafiti kadhaa wa majaribio kuhusu nishati ya kupikia mathalani mradi wa kutumia tungamotaka ambapo mifumo husika ilipelekwa katika maeneo 725 yaliyopo sehemu mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa Wakala umeshirikiana na kampuni za usambazaji gesi kufanya utafiti kuhusu uwezekano wa kuhakikisha nishati ya gesi inafikishwa katika maeneo ya vijijini kwa gharama nafuu ili wananchi waitumie kwa shughuli za kupikia.
Katika hatua nyingine, viongozi hao waliwahakikishia Wakuu wa Wilaya za Kibondo na Kakonko, ambao walikutana nao kwa nyakati tofauti kuwa maeneo yote ya kimkakati, hasa yanayohusisha masuala ya usalama yatapelekewa huduma ya umeme ili kuwezesha shughuli hizo kufanyika kwa ufanisi.
Awali, Mkuu wa Wilaya za Kakonko, Kanali Evance Malassa na wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza, kwa nyakati tofauti waliomba maeneo ya mpakani ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme, yapewe kipaumbele katika kufikishiwa nishati hiyo ili kuimarisha shughuli za kiusalama.
Pia, wakuu hao wa wilaya walipongeza jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na REA katika kusambaza umeme vijijini kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.
NA MWANDISHI WETU, KIGOMA





























