WANANCHI wametakiwa kujenga tabia ya kunywa Maji mara kwa mara hasa kipindi hiki cha uwepo wa ongezeko la Joto Kali linalotokana na kusogea kwa Jua la Utosi.
Ushauri huo kwa wananchi ni kutoka kwa Wataalamu wa Afya lengo likiwa ni kukabiliana na hali ya uwepo wa Joto kali.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, vipindi vya Jua la Utosi hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea Kusini na hali hiyo hujirudia mwezi Februari wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea Kaskazini.
Jua la Utosi kwa kawiada huambatana na hali ya Joto Kali kwa sababu Uso wa Dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na Jua kuliko maeneo mengine.
Viwango vya Joto vilivyoripotiwa katika maeneo mbalimbali ni vikubwa ambapo Mkoa wa Kilimanjaro umeripoti kiwango cha Juu cha Joto kilichofikia Nyuzi Joto 36.4 sawa na ongezeko la Nyuzi Joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba.
Kiwango cha Juu cha Joto Jijini Dar es Salaam kimefikia Nyuzi Joto 33.8 sawa na ongezeko la Nyuzi Joto 2.2.
Na MWANDISHA WETU





























