WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameagiza Wizara ya Maji kukaa pamoja na Mkandarasi M. A. Kharafi & Sons ili kukubaliana namna bora ya kukamilisha kazi zilizobakia katika utekelezaji wa mradi wa maji wa Same, Mwanga Korogwe ili kuhakikisha utekekeza wa mradi huo unafanyika kwa haraka.
Agizo hilo amelitoa Septemba 24, 2021, baada ya kukagua mradi huo unaotarajia kuhudumia zaidi ya wananchi 438,000.
Aidha, ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha vijiji vyote vinavyozunguka eneo la chanzo cha maji, eneo la Bwawa la Nyumba ya Mungu ilikowekwa miundombinu kuwa wanufaika wa kwanza wa mradi huo utakapokamilika.
Majaliwa amesema serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya maji safi na salama hivyo haitavumilia kuona mtu yeyote anakwamisha utekelezaji wa mradi.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema pamoja na kazi zingine mkandarasi huyo anatakiwa kuwezesha upatikanaji wa transforma kwa ajili umeme ambao utawezesha maji kufika kwenye mtambo wa kutibu maji na hatimae kusafirishwa kwenye matenki hadi kwa wananchi.
“Waziri Mkuu. Nikuhakikishie kuwa, Rais aliniambia nikimzengua tunazenguana. Sitakuwa tayari kukuzingua wala kumzingua Rais wangu. Wizara ya maji tuko tayari kukamilisha mradi huu.” Amesema Aweso.
Mradi wa maji wa Same, Mwanga hadi Korogwe unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 262 na utakapokamilika utahudumia wananchi wapatao laki 438.





























