TAKRIBAN Kaya 40,740 nchini, zinatarajiwa kunufaika kwa kuwezeshwa kiuchumi kupitia fedha za mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ikiwa ni hatua za kuondoa athari zilizosababishwa na ugonjwa wa virusi vya corona (Uviko-19).
Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga, alisema fedha hizo sh. bilioni 5.5 ambazo ni sehemu ya mkopo wa sh. trilioni 1.3 ambazo IMF iliikopesha Tanzania kwa masharti nafuu.
Alieleza fedha hizo zilizoidhinishwa kwa TASAF, zitatumika kuondoa athari za kiuchumi zilizochochewa na Uviko-19 kwa kaya za walengwa wa mfuko huo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, fedha hizo zitaelekezwa katika utoaji wa ruzuku na utekelezaji wa miradi ya ajira za muda kwa kaya za walengwa ili kupata kipato cha kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Fedha hizo zitapunguza athari za Uviko-19 na kuongeza rasilimali na miundombinu itakayotumika na jamii yote katika mitaa, shehia na kupitia fedha hizo kaya za walengwa 40,740 zitanufaika,” alisema.
Alibainisha kaya hizo ni zenye uwezo wa kufanya kazi na zinazoishi katika maeneo ya mijini na zitafanya kazi katika miradi ya kijamii na kulipwa ujira wa wastani wa sh. 135,000 kwa kaya.
Alisisitiza shabaha ya uwezeshaji huo ni kufufua au kuimarisha shughuli za kukuza uchumi wa kaya hizo, zilizoathiriwa na Uviko-19.
“Serikali imedhamiria kuwaondoa katika umasikini kwa kuwapatia ruzuku za kujikimu, ajira za muda na kuwaongezea ujuzi, maarifa na elimu ya ujasiriamali ili wakidhi mahitaji yao,” alisema.
Alisema utolewaji wa fedha hizo ni uthibitisho wa dhamira ya serikali katika kuwajali wananchi hususan wanaoishi mazingira duni.
Mkurugenzi huyo alisema TASAF inatekeleza mpango wa kunusuru kaya za walengwa katika Halmashauri 184 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba.
Na JUMA ISSIHAKA





























