BODI ya Usajili ya Wahandisi inatarajia kuwasajili wahandisi zaidi ya 632, katika siku ya maadhimisho ya Wahandisi Tanzania itakayotarajiwa kufanyika Septemba 2, mwaka huu, jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya maadhimisho hayo Prof. Bakari Mwinyiwiwa katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dodoma.
Amesema malengo ya kuadhimisha siku hiyo pamoja na kuiwezesha jumuiya ya kihandisi kuuonyesha uuma wanachokifanya kuleta maendeleo ya nchi na kutambua wahandisi na makampuni yao.
Amesisitiza kuwa, wageni watakaoshiriki wanatarajiwa kutoka katika nchi mbalimbali kama Uganda, Misri, Afrika Kusini, DRC, Rwanda, Botswana na Kenya, na kuongeza kutakuwa na kiapo kitakachowahusisha wahandisi zaidi ya 632 watakaotunukiwa taaluma hiyo.
“Wahandisi wataaluma watakula kiapo cha utii ili kuhakikisha wanawajibika vyema katika taaluma zao mtambue tu kuwa bodi ilianzisha utaratibu huu kwa wahandisi wote kula kiapo na itakua ni mwiko kwako kukiuka maudhui ya kiapo hichi’” amesema Profesa.
Mkutano huo pia utaendana na majadiliano ya kitaaluma ambayo yatawasilishwa na mada mbalimbali kutoka kwa walimu pamoja utoaji wa tuzo kwa wahandisi watakaohitimu katika vyuo vikuu, Taasisi iliyotia fora katika maonyesho ya biashara, Uchukuzi na utoaji huduma za kitaaluma.
Na. Benedict Mwasapi





























