MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imemuamuru Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Isack Kihwili, kuilipa zaidi ya sh. bilioni 145.9 kampuni ya Coast Textiles Limited.
Amri hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Jaji Amir Mruma ni utekelezaji wa hukumu ya Mahakama iliyotolewa takriban miaka saba iliyopita dhidi ya FBME Bank Limited.
Jaji Mruma alitoa amri hiyo kwa mlalamikiwa Mkurugenzi wa DIB aliyeteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwa Mfilisi wa Benki ya FBME, baada ya kuridhia maombi ya utekelezaji wa hukumu yaliyowasilishwa na mwombaji Coast Textiles Limited.
Alisema mwombaji ana haki ya kutekeleza hukumu ya mahakama, hivyo anakubaliana na ombi hilo na kuamuru mfilisi wa benki ya FBME atimize amri hiyo.
Mlalamikiwa huyo kupitia hati yake ya kiapo, ili kuonyesha sababu za kutaka kutupiliwa mbali kwa ombi hilo, alidai kwa kuwa benki ya FBME ilikuwa inafilisiwa, utekelezaji au ukamataji wowote hauwezi kutekelezwa dhidi ya mali zake, hatua hiyo haiwezi kufikirika na ni kinyume cha sheria.
Katika uamuzi wake, Jaji Mruma alibainisha hakuna ushahidi wa kutosha uliowasilishwa kuonyesha benki ya FBME ilikuwa mfilisi na hakuna mahali popote palipoonyeshwa taasisi hiyo ya kibiashara haina uwezo wa kulipa madeni kwa wadai wake.
Alisema alibainisha zaidi hakuna sababu zilizotolewa na mfilisi kuonyesha ni kwa nini benki husika ilifungwa na baada ya hapo kunyang’anywa leseni yake ya uendeshaji.
Jaji huyo alisema ilibainika benki ya FBME ilifungiwa Mei 8, 2017 wakati ambapo Mahakama ilikuwa tayari imeshatoa hukumu ya shauri hilo kwa upande wa Coast Textile Limited.
“Mahakama ndiyo yenye amri ya mwisho katika utoaji haki, hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo haiwezi kuchunguzwa au kuorodheshwa na mfilisi. Ninakataa kutoa uamuzi kwamba mwasilishaji maombi hawezi kutekeleza hukumu ya mahakama,” alisema.
Kampuni hiyo ya Coast Textiles Limited, iliwasilisha maombi ya utekelezaji hukumu ikidai sh. 145,946,500,641 zilipwe na DIB kwa kuwa ilichukua ufilisi wa benki ya FBME na iwapo itashindwa, Mkurugenzi wake awajibishwe kwa kulipa fedha hizo.
Kampuni hiyo ilikuwa mahakamani kwa takriban miaka 24 tangu tangu 1997, ikitafuta haki zake dhidi ya benki ya FBME, ambayo baadaye ilichukuliwa na BoT ili kuwalinda wateja wa Kitanzania, baada ya kuhusishwa na makosa ya utakatishaji fedha huko Cyprus.
Mahakama Kuu ilitoa hukumu katika kesi hiyo Julai 27, mwaka 2015, ambayo ni zaidi ya miaka sita, amri hiyo haijatekelezwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Coast Textiles Limited, Sudhir Lakhanpal, alishawahi kuuomba Ubalozi wa India kuingilia suala hilo, juhudi hizo hazikuzaa matunda hatua iliyomlazimu kuwasilisha maombi ya kukazia hukumu iliyotolewa.
Na REHEMA MOHAMED



























