SERIKALI ya nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ya Abu Dhabi, imeahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kiuchumi na kijamii baina yake na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Ahadi hiyo imetolewa mjini Abu Dhabi na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Rais, Sheikh Mansour bin Zayed Al Nanyan, baada ya kupokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, uliowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba.
Akizungumza baada ya mazungumzo ya faragha, Dk. Mwigulu alisema Sheikh Mansour ameahidi kutuma ujumbe maalum nchini kwa ajili ya kuangalia miradi ya kimkakati inayotokelezwa na mingine mipya kwa lengo la kutoa fedha.
Mwigulu aliitaja miradi iliyowasilishwa kwa Serikali ya Abu Dhabi ni uendelezaji wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Nishati ya Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere, ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, kilimo, uvuvi na elimu.
“Katika sekta ya elimu tumejenga madarasa mengi, tumejenga vituo vya afya vingi na vingine viko vijijini, lakini hatujajenga nyumba za watoa huduma wanaotakiwa kufanyakazi katika maeneo hayo,” alisema.
Alisema wamejadiliana na Sheikh Mansour kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini kwani Tanzania ni lango la kibiashara kwa nchi zisizozungukwa na bahari ambazo zikitumiwa vizuri zitaifanya nchi ipae zaidi kiuchumi.
“Maeneo mengine tuliyojadiliana ni namna ya kuitumia na kuishirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) kuleta faida kwa pande zote mbili,” alieleza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Jamal Kassim Ali, alisema mkutano wao na Naibu Waziri Mkuu wa Abu Dhabi, uliangazia pia masuala ya Zanzibar ambapo miradi kadhaa ya kimkakati inayotaka ufadhili iliwasilishwa.
Aliitaja miradi hiyo ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Manga Pwani kwa njia ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi, ujenzi wa nyumba za makazi za gharama nafuu zipatazo 10,000 kwa watumishi wa umma na wananchi pamoja na uchimbaji wa mafuta na gesi.
“Zanzibar tuna fursa katika masuala ya uchumi wa buluu ikiwemo uchimbaji wa mafuta na gesi, masuala ya uvuvi, utalii na wenzetu wamepiga hatua katika maeneo hayo, tukishirikiana nao tutapiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii,” alisema.
Aliishukuru Abu Dhabi kwa kuendeleza ushirikiano na Tanzania hususan visiwa vya Unguja na Pemba ambapo nchi hiyo ya Kiarabu ilifadhili ujenzi wa Hospitali ya Wete-Pemba.
Aliahidi kuwa tayari kuendeleza ushirikiano huo katika miradi mipya iliyowasilishwa kwao.
Na Benny Mwaipaja, Abu Dhabi





























