WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, ameeleza kusikitishwa na kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Mkoani Tabora.
Pia, amesema hajaridhishwa na hali ya uandikishaji wa wanafunzi wa madarasa ya awali na wale wanaoanza darasa la kwanza katika wilaya hiyo.
Waziri Ummy alionyesha hali hiyo wakati wa ziara yake wilayani humo na kupokea taarifa iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Advera Bulimba.
Alisema kuanzia mwaka 2017 kiwango cha ufaulu wa wanafunzi waliohitimu darasa la saba kinashuka mwaka hadi mwaka. Mwaka 2017 ufaulu ni asilimia 72, 2018 ilikuwa asilimia 63, mwaka 2019 ulikuwa asilimia 65, huku mwaka 2020 ufaulu ulikuwa asilimia 58 na mwaka 2021 ulikuwa asilimia 56.
“Takwimu hizi haziridhishi kabisa lazima mfanye uchunguzi wa kina kufahamu sababu ya kuporomoka kitaaluma namna hii. Hili halivumiliki mnatakiwa kufanya kitu cha ziada kuhakikisha mnaongeza kiwango cha ufaulu,” alisisitiza.
Ummy alinyooshea kidole idadi ndogo ya wanafunzi wanaoandikishwa kuanza shule ya awali na darasa la kwanza.
Aliweka bayana kuwa hali ya uandikishaji wa wanafunzi katika darasa la awali kwa mwaka 2021/22 ni asilimia 17 na kwa wanafunzi wanaotakiwa kuanza darasa la kwanza ni asilimia 14.
“Kwa nini watoto wanaoandikishwa kuanza madarasa ya awali na la kwanza ni wachache kiasi hiki, ina maana hamhamasishi jamii kuandikisha watoto shule. Niwatake sasa kila mtu kwa nafasi yake aamke na kwenda kuhamasisha wananchi kupeleka watoto shule na takwimu zibadilike,” aliagiza.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Buriani, alisema kwa hali ilivyo sasa watatumia njia zote kuhakikisha watoto wanaandikishwa shule kama vile kupitisha gari la matangazo, kutumia mikutano na mikusanyiko kuhamasisha jamii na mwishoni kufanya msako nyumba kwa nyumba kubaini kama kuna mtoto mwenye umri wa kwenda shule ambaye hajaandikishwa.
Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Sistaimelda Lubengon, alisema mwamko duni wa jamii na utoro wa mara kwa mara wa wanafunzi ni baadhi ya sababu zinazochangia kuporomoka kwa ufaulu katika halmashauri hiyo.
NA MWANDISHI WETU, Tabora





























