MKAZI wa Kijiji cha Buriba, Sinda Mseti, amejinyonga hadi kufa, kwa kinachodaiwa kutoridhika na uamuzi wa mama yake Maria Chacha kumzuia kuuza kiwanja.
Polisi Kanda Maalumu Tarime Rorya, imethibitisha kutokea kwa tukio hilo, baada ya kijana huyo kutoelewana na mama yake kuhusu uamuzi wake wa kutaka kuuza kiwanja.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Tarime Rorya, ACP William Mkonda, alisema Mseti alitaka kuuza kiwanja hicho, ndipo mama yake alipinga hatua hiyo, hivyo aliamua kwenda kujinyonga jirani na nyumbani kwao.
Alisema wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua uamuzi usiokuwa na tija, badala yake inapotokea kutoelewana katika familia, washirikishe ndugu na watu wa karibu.
Mkonda alisema hatua ya kushirikisha familia, inatasaidia jamii kupata suluhu na inaposhindikana masuala hayo wayafi kishe katika vyombo vya sheria ili haki itendeke.
Wakati huo huo, wakazi wa Kijiji cha Gwitiryo, Kata ya Gwitiryo, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuvamia na kumkata mapanga Charles Marwa na kumnyang’anya sh. 270,000. Watuhumiwa hao Charwi Chacha na Siseri Nyakerenge, wanatuhumiwa kutenda kosa hilo, mwishoni mwa wiki usiku, wakati Marwa alipokuwa akirejea nyumbani kwake.
“Wakati Charles Marwa alipokuwa anarejea nyumbani kwake, nje ya lango la nyumba yake alivamiwa na kundi la watu hao ambao aliwafahamu na kuanza kumkatakata na kumpora fedha zake.”
“Watuhumiwa wanatarajiwa kufi kishwa mahakamani wakati wowote. Natoa onyo kwa watakojihusisha na vitendo vya uvunjivu wa amani wakati wa sikukuu za krismasi na mwaka mpya, jeshi limejipanga kukabiliana na uhalifu,” alionya.
Na SAMSON CHACHA, Tarime



















