BALOZI wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema wakati Tanzania ikielekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), nchi yake inajivunia ushirikiano wa mafanikio uliopo baina ya nchi hizo.
Amesema katika kipindi hicho, nchi yake kupitia Chama cha Kikomonisti cha Watu wa China (CPC) imeendelea kuimarisha umoja na mshikamano na Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari, kwa njia ya mtandao, Balozi Chen alisema wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, CPC mwaka huu imetimiza miaka 100 ya mageuzi ya kiuchumi, huku ikiwa imepiga hatua kubwa ambazo anaamini Tanzania inaweza kuzifikia.
Kwa mujibu wa Balozi Chen, zipo hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Tanzania ambazo anaamini zinaweza kuipeleka nchi katika hatua kubwa ya kiuchumi, huku akisisitiza katika kipindi cha miaka 100 ya mageuzi ya China, nchi hiyo ilijikita katika kuwajibika, kujali watu, kutanguliza uzalendo na kufanya kazi kwa bidii kwa kila mwananchi.
“Tunaamini Tanzania inayo nafasi ya kufanya makubwa zaidi katika maendeleo. Tunaahidi kutoa ushirikiano zaidi ili kufikia malengo ya ustawi wa jamii kwa pande zote mbili ikiwamo kiuchumi, kiutamaduni na kidilpomasia,” alisema.
KUHUSU MKUTANO WA DAKAR
Balozi Chen alisema mkutano wake huo na waandishi wa habari, ulilenga kutoa mrejesho kuhusu mkutano mkubwa wa kimataifa wa kuimarisha ushirikiano baina ya China na nchi za Afrika, uliofanyika Dakar, Senegal.
“Mkutano huu ambao ulikuwa jukwaa maalumu la kujadili ushirikiano na kuweka mikakati ya kuimarisha maendeleo, umefanyika kwa mafanikio makubwa. Nchi takriban 53 zimeshiriki kwa kutuma viongozi waandamizi wa ngazi za juu serikalini.
“Tanzania iliwakilishwa na Balozi Mulamula (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Liberata Mulamula) ambaye amekuwa na ushiriki mzuri kwa kushirikiana na timu aliyoambatana nayo,” alisema Balozi Chen akielezea mkutano huo uliofanyika kuanzia Novemba 29 hadi 30, mwaka huu.
Na MWANDISHI WETU




























