JARIDA maarufu duniani la Forbes la nchini Marekani, limemtangaza Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa miongoni mwa viongozi bora 100 wanawake wenye ushawishi mkubwa duniani.
Katika orodha hiyo wapo viongozi wanawake 19 kutoka mataifa mbalimbali duniani akiwemo Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris.
Wengine ni wataalamu wabobezi wa masuala ya tiba za kibaiolojia pamoja na wanawake wakurugenzi watendaji kutoka kampuni zilizoweka rekodi ya kuingiza mapato ya zaidi ya dola trilioni 3.3.
Wanawake wengine walioingia katika orodha hiyo ni Reese Witherspoon ambaye ni mwigizaji, mtayarishaji wa vipindi na mjasiriamali, Mwenyekiti wa Kampuni ya Hong kong Exchange na Clearing, Laura Cha na Rosalind Brewer ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Walgreens.
Samia aliingia katika siasa kama mwanachama wa CCM, Juni 10, 1987. Aliingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2000 katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar akiwa Mwakilishi wa Viti Maalumu.
Na MUSSA YUSUPH





























