KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amewahakikishia wanachama na wananchi, Chama kitatekeleza yaliyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa kiwango chenye tija.
Chongolo ameyasema hayo, alipozungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika maeneo tofauti ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, Wilaya za Wete na Micheweni, akiwa katika ziara ya siku mbili akiambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).
“Niwahakikishe Chama Cha Mapinduzi kimejipanga, kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020- 2025 ambayo imeahidi mambo mbalimbali yakiwemo maji, umeme, barabara, miundombinu ya elimu…imeahidi mambo mengi ndani yake, yanatekelezwa kwa kiwango chenye tija.
“Ndiyo maana mnaona tunapita kama hivi. Kazi yetu sisi ni kupita kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa tulichokiahidi kwenu, na ndio kazi tunayoifanya sasa hapa Pemba kwa siku mbili,” alisema Chongolo akizungumza na katika Kijiji cha Taifu.
Akitoa salamu na ujumbe wa viongozi wakuu wa serikali, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa wananchi wa wilaya ya Wete , Chongolo alieleza kuwa;
“Rais Samia ameniambia niwahakikishie ataendelea kushirikiana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi kupambana kwa ajili ya miradi na changamoto zinazowakabili ili ndani ya miaka mitano wilaya ya Wete na Pemba kwa ujumla kuwe na mabadiliko makubwa ya maendeleo.”
Chongolo alieleza kuwa Rais Dk. Mwinyi alimtuma salamu zake kwao, awaeleze wananchi kuwa;
“Anajua changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa baadhi ya maeneo ya Wete na amewahakikisha maji yatawafikia wananchi wote kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 kama ilivyo kwa Kijiji cha Taifu kilichokuwa na uhaba wa maji kwa zaidi ya miaka 14 na sasa maji yanapatikana ya kutosha.”
Katika hatua nyingine, Chongolo amewataka wananchi kuwa macho kupita na kukagua miradi ya ujenzi wa hospitali za wilaya unaoendelea katika wilaya zote za Kaskazini Pemba ikiwemo Wete ambapo zaidi ya sh. bilioni nne zimepelekwa na ujenzi unaendelea.
Mbunge wa Jimbo Gando, Salum Musa Omary amekishukuru Chama na serikali kuendelea kushusha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ukiwemo upatikanaji wa maji katika Kijiji cha Taifu ambacho kilikuwa na uhaba kwa zaidi ya miaka 14.
Chongolo akikagua ujenzi wa Hospitali ya Wete inayogharimu sh. bilioni 4.71 ambapo aliwataka vijana kuchangamkia fursa za mafunzo ya ufundi na ujuzi zinazotolewa na serikali kujipatia kipato kwa kushiriki ujenzi wa miundombinu ukiwemo wa madarasa na hospitali unaoandela katika maeneo mbalimbali Pemba.
Akizungumza na wana CCM katika kikao cha Shina Namba 1, Tawi la Kiuyu, Kigongoni, Wilaya ya Wete, alitoa wito kwa wanachama wa CCM wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa ndani wa Chama mwaka huu, lazima wajipime na wajue wajibu wa uongozi ndani na nje ya Chama, badala ya kusukumwa na tamaa binafsi kutaka uongozi, bali kutumikia watu.
Chongolo aliwataka wananchi kuhamasishana kujitokeza kwa wingi katika sensa ya watu na makazi itakayoanyika mwaka huu.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mattar Zahoro Mattar alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kufanya Pemba kuwa mojawapo ya maeneo ya kimkakati ya uwekezaji kukuza Uchumi wa Buluu.
NA MWANDISHI WETU, PEMBA




























