SERIKALI imesema tume iliyoundwa kuchunguza upandaji bei za bidhaa za vinywaji baridi nchini, imebaini wasambazaji wa bidhaa hizo walipandisha bei kinyemela na siyo wamiliki wa viwanda.
Kutokana na hali hiyo, imewaagiza maofisa biashara nchini kufanya ukaguzi wa bei za bidhaa zinazouzwa katika maeneo yao, kisha wawasilishe ripoti kupitia ofisi za mikoa na wilaya, ili hatua zichukuliwe kuondoa malalamiko ya wananchi ya kupanda kwa bei za bidhaa kiholela.
Waziri wa UwekezajI, Biashara na Viwanda, Dk. Ashatu Kijaji, ametangaza hilo muda mfupi baada ya kumaliza kutembelea kiwanda cha kutengeneza vinywaji baridi na bidhaa zingine cha Jambo Group, mjini Shinyanga, ambapo alizitaka taasisi zote zilizoko chini ya wizara yake ziwajibike.
Dk. Kijaji ameziagizaTume ya Ushindani (FCC), Wakala wa Vipimo (WMA) na nyinginezo zihakikishe zinafanya kazi kwa mujibu wa utaratibu ikiwemo kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa viwandani hazipandishwi bei kiholela.
“Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara, wasambazaji wa bidhaa kupandisha bei hovyo kwa maslahi yao, ushindani na soko huria upo siyo kwa sababu ya kufanya hivyo, sheria zipo, mamlaka zipo kuhakikisha mwananchi anatendewa haki,” alieleza.
Akitoa ripoti ya tume aliyoiunda kuchunguza upandaji wa bei za bidhaa mbalimbali kuanzia vinywaji baridi, alisema tume hiyo imegundua viwanda vya Coca Cola, Pepsi na viwanda vingine havikupandisha bei, bali kuna wasambazaji wa kati ambao walikuwa chanzo cha upandaji wa bei.
Waziri huyo aliwataka wafanyabiashara kujua kuwa uwepo wa soko huria hauna maana kwamba serikali haitosimamia soko na kuona mambo yanakwenda ndivyo sivyo katika biashara, haitavumilia na aitachukua hatua stahiki.
Alisema tume hiyo ilibaini changamoto ya uhaba wa sukari ya viwandani iliikumba viwanda kwa sababu ya soko la dunia kuyumba kutokana na wa athari za Uviko-19.
“Nawapongeza wamiliki wa viwanda vya vinywaji baridi kwa ubunifu wao baada ya kukosekana makasha ya sukari, walianzisha utaratibu wakuagiza sukari hiyo na tayari serikali imeweka utaratibu wa kuomba vibali vya kuagiza sukari hiyo kwa mtandao ili kuhalakisha upatikanaji wa bidhaa hiyo,” alieleza.
Mmiliki wa kiwanda cha Jambo, Salumu Khamisi, aliipongeza serikali kwa hatua inazochukua kulinda viwanda vya ndani ambapo alisema kampuni yake haikupandisha bei za vinywaji vyao ili kutowaathiri watumiaji.
Salumu aliwataka wafanyabiashara na wasambazaji kufuata bei elekezi za viwanda wanakochukulia bidhaa, kwani serikali ipo na sheria zipo kwa ajili ya wale wanaokiuka taratibu.
Na Chibura Makorongo, Shinyanga





























