MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein, amewataka wanachama wa CCM, kutofanya makosa ya kuwachagua viongozi wa Chama katika uchaguzi wa ndani unaotarajia kufanyika mwaka huu.
Dk.Shein alisema wanachama wa CCM hawatakiwi kufanya makosa ya kuchaguana katika uchaguzi huo kwa kubaguana kwa majina, badala yake wawachague viongozi kwa kuzingatia uwezo na sifa.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizindua ugawaji wa kadi mpya za CCM za kielektroniki Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar.
Alisema kuna haja ya kuhakikisha viongozi wanachaguliwa kwa kuzingatia sifa za uwezo wa utendaji na ukereketwa wa CCM kwa kukifahamu Chama na misingi yake.
Dk.Shein alisema kuna kazi kubwa ya kuwapata viongozi watakaongoza miaka mitano ijayo, hivyo kuna haja ya kuwachagua watu ambao wapo tayari kukitumikia chama.
Dk.Shein alisema mabadiliko yanayotokea duniani ndio kimeifanya CCM kuanza kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kadi mpya za kieletroniki.
Alisema mfumo wa TEHAMA una mafanikio makubwa na umadhubuti wake na kwamba kuna sababu ya kuanza kuingia kwenye mfumo huo ikiwemo matumizi ya kadi za kietroniki.
Makamu huyo mwenyekiti alisema matumizi ya mfumo wa TEHAMA una faida kubwa ambapo taarifa za mwanachama zitabakia hata kama kadi yake ataipoteza.
Alisema misingi hiyo ya demokrasia ni pamoja na kuhakikisha inasimamia makusanyo ya mapato ndani ya Chama kuwatumikia wananchi na ufanyaji wa kazi kwa usanifu.
Dk.Shein alisema wanachama wa CCM wanapaswa kuunga mkono serikali mbili kutokana na kuwa Chama kinaongoza serikali hizo ikiwemo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mjumbe mstaafu wa Kamati Maalumu ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais mstaafu, Balozi Seif Ali Idd, alisema kadi mpya za CCM za kieletroniki ni nzuri kutokana na kuwa ni rahisi kutunzika.
NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR





























