WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameipongeza sekta binafsi kwa namna inavyoshiriki katika kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kutoa fursa za ajira kwa Watanzania kupitia kampuni na mashirika mbalimbali.
Ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki, katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Jumuia ya Watendaji Wakuu wa Kampuni na Mashirika (CEO Roundtable of Tanzania) katika ukumbi wa hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa, moja ya mafanikio makubwa ni kuongezeka kwa ajira kutoka milioni 20.5 mwaka 2014 hadi milioni 24.1 mwaka 2020/2021 na kuongezeka kwa ajira katika sekta isiyo rasmi kutoka asilimia 22 mwaka 2014 hadi asilimia 29.4 mwaka 2020/2021.
Alisema licha ya changamoto ya UVIKO-19, Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika sekta nyingine za kiuchumi na kutoa ajira katika sekta ya kilimo, hali ambayo inaashiria mwelekeo mzuri wa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, unaolenga kuwa na asilimia 60 ya ajira katika kilimo ifikapo mwaka 2025/2026.
“Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uwekezaji, biashara na kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hatua hizo, zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji nchini hasa kutoka nje ambao kati ya Machi na Agosti, mwaka huu, ulifikia takriban dola za Marekani bilioni tatu,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Rais Samia, ameendelea kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara na anaamini kupitia mkutano huo watatoa ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji.
Aliongeza kuwa, serikali ina matarajio na sekta binafsi kuendelea kuunga mkono jitihada za kupambana kupunguza hewa ya ukaa na matumizi ya plastiki.
“Ongezeni uwekezaji kwenye miradi ya matumizi ya nishati mbadala, ustawishaji wa misitu na utunzaji wa mazingira na usafirishaji kwa kutumia teknolojia za kisasa zisizozalisha hewa ya ukaa,” alisema na kuongeza:
“Nitoe wito kwenu, mwendelee kuwaita wawekezaji waje nchini na kuwekeza katika sekta mbalimbali za kilimo, utalii na nishati.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa aliitaka sekta binafsi iweke kipaumbele na kuzingatia usawa wa kijinsia katika utoaji wa ajira hususan kwa wanawake, ili kuunga mkono jitihada za serikali.
Alieleza kuwa, katika mwaka 2020/2021, ukosefu wa ajira kwa wanawake, umeonekana kuwa juu zaidi ikilinganishwa na wanaume, ambapo wanawake wasiokuwa na ajira wanafikia asilimia 12.7 ilhali wanaume ni asilimia 5.8.

“Katika mipango yenu ya sasa na baadaye, toeni kipaumbele kwenye mikakati ya kuwainua wanawake katika shughuli za uchumi na hivyo, kumuunga mkono kwa vitendo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuleta usawa wa kijinsia kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema.





























