WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ya Awamu Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuchukua hatua kuboresha mazingira ya kujiajiri kwa wananchi hususan vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Dk. Nchemba alitoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akiwatunuku tuzo wahitimu katika mahafali ya 35 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini.
Alisema kwa sasa, soko la ajira linakabiliwa na changamoto, hivyo lazima wahitimu wanaomaliza katika vyuo mbalimbali nchini, wafikirie zaidi kujiajiri kuliko kuajiriwa.
Alifafanua kuwa, miaka ya zamani, taasisi zilikuwa zikitafuta wahitimu na kuwafuata hata majumbani ambapo mhitimu alikuwa akipata ajira mara moja au kabla hajahitimu.
“Dhana hii sasa imepitwa na wakati, kuna haja ya jamii ya sasa kuhama katika mawazo waliyorithishwa na wazazi wetu, zamani waajiri walikuwa wanatafuta wa kuwaajiri, lakini sasa waajiriwa wenyewe ndio wanaotafuta ajira,” alisema.
Alibainisha kuwa, katika kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imeendelea kuziagiza halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kutoa mikopo ya masharti nafuu.
“Natambua kuwa, mtazamo wa kusoma elimu ya juu ili kujiajiri, unaweza usiendane na matarajio siyo ya wahitimu wetu, bali hata ya wazazi, walezi na jamii kwa sehemu kubwa.
“Mathalani, pamoja na uhalisia kuwa katika nchi yetu kati ya vijana 100 wanaoingia kwenye soko la ajira, ni vijana saba tu ndio wanapata ajira katika sekta rasmi, sehemu kubwa ya jamii imeendelea kuwa na imani kuwa kijana wao aliyehitimu masomo ya elimu ya juu, atapata ajira ya mshahara,” alisema.
Alisema mtazamo huo hasi wa jamii kuhusu kujiajiri, unafifisha ari ya vijana kuingia katika tasnia ya kujiajiri kwa kujiamini.
Waziri huyo alisema katika kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini, serikali imepunguza urasimu katika uanzishaji wa biashara, utoaji leseni na vibali kutoka mamlaka mbalimbali za udhibiti.
Alieleza kuwa, serikali imeendelea kutekeleza sera mbalimbali za fedha na nyinginezo ambazo zimewezesha benki za biashara kupunguza riba za mikopo, hivyo kupunguza gharama za mitaji.
Alikielekeza chuo hicho, kuendelea kuongeza wigo wa huduma za utafiti ambazo ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Awali, Mkuu wa Chuo cha Mipango, Profesa Hozen Mayaya, alisema chuo kimeanzisha Kituo cha Ujasiriamali na Ubunifu ambacho kinatoa fursa kwa vijana wenye maono na ndoto za ujasiriamali kulelewa ili kuweza kutimiza ndoto zao.
Alisema kituo hicho kitakuwa chachu katika kuendeleza mawazo na ubunifu walionao wanafunzi na hatimaye wanapohitimu mafunzo yao, waweze kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Profesa Mayaya alitaja idadi ya wanachuo waliohitimu katika mahafali hayo ya 35 kuwa ni 5,482, katika kozi mbalimbali wakiwemo wanaume 2,297 na wanawake 3,185.
Na Happiness Mtweve, Dodoma




























