KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael, ameitaka Makumbusho ya Taifa kutumia fedha za miradi inayofadhiliwa na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 kama zilivyokusudiwa kwa maendeleo endelevu.
Dkt. Francis Michael, ametoa wito huo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua Mradi wa Uboreshaji wa Kijiji cha Makumbusho wa kukuza utalii wa Kiutamaduni Kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Pamoja na kuipongeza Makumbusho ya Taifa kwa kazi nzuri inazozifanya katika uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni, amesisitiza fedha za miradi hiyo zitumike kama zilivyopangwa ili kuleta matokeo chanya ya malengo ye fedha hizo.
“Nitoe maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa kuhakikisha anasimamia miradi hii kikamilifu ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa, kwa kuzingatia umuhimu wa Kijiji cha Makumbusho kwa Jamii, Wizara na Serikali kwa ujumla” amesema Dkt Michael.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga, alieleza kuwa, fedha zilizotolewa kwa Kijiji cha Makumbusho zitatekeleza miradi ya Ujenzi wa Nyumba za Asili kwa kufuata Ramani ya Tanzania; Ujenzi wa maumbo ya sura ya nchi, kuakisi Ramani ya Tanzania (Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria); Uboreshaji wa Bohari na Maabara za Mikusanyo na Uboreshaji mandhari ya nje ya Kijiji ili kuleta mvuto shawishi kwa wapita njia na kuboresha onesho la kazi za sanaa za mikono.
“Tunatoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya utalii nchini.” Amesema Dkt Lwoga.
Na Mwandishi wetu





























