SIKU moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kukamilisha ziara yake nchini Ufaransa, wataalamu mbalimbali wa masuala ya uchumi wa bahari, wanasiasa na balozi, wameonyesha matarajio makubwa ya mafanikio yatakayopatikana kutokana na ziara hiyo.
Miongoni mwa faida zilizotajwa kutokana na ziara hiyo ya Rais iliyomwezesha pia kuhutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Rasilimali Bahari Duniani ‘One Ocean Summit’ nchini humo, ni pamoja na kufungua fursa za uwekezaji.
Akizungumza na UHURU kwa njia ya simu, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Samwel Shelukindo, alisema ziara ya Rais Samia nchini humo ambayo imetokana na mwaliko wa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, imekuwa na tija kwa diplomasia ya nchi hizo katika uchumi na uwekezaji.
Alisema kutokana na ziara hiyo, kampuni 60 kutoka nchini Ufaransa zimeitikia wito na zipo tayari kwa ajili ya uwekezaji Tanzania.
“Imekuwa ziara nzuri kuanzia mapokezi na mafanikio yaliyofikiwa, Ufaransa inaongoza kwa kuleta watalii wengi nchini Tanzania na inaenda kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya uwekezaji,” alisema.
Balozi Shelukindo aliongeza kuwa, katika ziara hiyo, wakuu hao wa nchi mbili hizo, kwa pamoja walikubaliana mambo makubwa kadhaa, ikiwa ni pamoja na utayari wa Ufaransa kuisaidia Tanzania kupambana na uhalifu katika bahari kuu ili kuimarisha uchumi wa buluu.

Aidha, alieleza kuwa uchumi wa buluu ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, hivyo Rais Macron amemuahidi Rais Samia kuwa nchi yake itafanya uwekezaji mkubwa katia sekta hiyo, ikiwemo kulinda uhalifu unaoweza kufanyika katika bahari kuu.
Alisema kati ya mikataba iliyotiwa saini kwa nchi hizo mbili ni pamoja na makubaliano kati ya Benki ya Kilimo Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.
“Mkataba huo ni wa zaidi ya Euro milioni 80, ambapo utasaidia sekta ya kilimo, huku mkataba wa ukarabati wa mindombinu na uwanja wa ndege wa terminal II, ikiwa ni muhimu ili kuimarisha sekta ya uchumi nchini,” alisema.
Alieleza kuwa, baada ya ziara hiyo, Watanzania watarajie wawekezaji wengi kutoka Ufaransa kuanzia Mei, mwaka huu.
Balozi Shelukindo alisisitiza kuwa, mikataba hiyo itaanza utekelezaji wake hivi karibuni baada tu ya kutiwa saini, kwa kuwa ilishafanyiwa tathimini.
WATAALAMU UCHUMI BAHARI
Kwa upande wa wataalamu mbalimbali wa uchumi kupitia rasilimali za bahari, walisema ziara hiyo na ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa ‘One Ocean Summit’ walisema utaongeza ushirikiano na mataifa mengine katika kulinda rasilimali bahari na kufanyika tathimini ya uwezo wa kitaifa kukabiliana na changamoto za uchafuzi, hivyo kuundwa mkakati ya kukabiliana nazo.
Akizungumza na UHURU, Februari 15, 2022, mtaalamu wa sayansi ya mazingira, Profesa William Mwegoha, alisema sera ya mazingira nchini inatambua umuhimu wa kushirikiana na mataifa mengine katika masuala ya mazingira.
Alieleza kuwa uchafuzi wa mazingira, hususan bahari, hauna mipaka, huvuka kutoka nchi moja kwenda nyingine, ndiyo maana kunafanyika mijadala mbalimbali ili kutatua changamoto hizo kuanzia ngazi za kidunia.
“Nchi siyo kisiwa, bali ipo kwenye mfumo wa kidunia, kwa hiyo majadiliano mengi lazima yataanza katika hatua za kidunia ili kujenga ushirikiano katika mapambano na changamoto za mazingira,” alisema.
Alifafanua kuwa ni muhimu kwa nchi kushiriki, kwa kuwa athari zinazotokana na shughuli za binadamu, huenda zikaanzia nchi yoyote na kusambaa hadi katika taifa lingine.
“Kwa hiyo ile mikakati inayowekwa kwa ajili ya kukabiliana na masuala hayo lazima na sisi (Tanzania) tuwe tunashiriki kujenga au kulinda maslahi yetu,” alisema.

Alisema maana ya Tanzania kushiriki mkutano huo ni kwamba inafanyika tathimini ya uwezo wa kila nchi kukabiliana na changamoto hizo, katika upande wa rasilimali na utaalamu.
Alibainisha katika mkutano huo, hufanyika majadiliano ya kukubalina namna ya kufanya na nchi gani inahitaji msaada upi kukabili changamoto ipi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Utafiti katika Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Amos Majule, alisema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni muhimu kutokana na uwepo wa mikataba ya kimataifa kuhusu bahari ambayo nchi imetia saini.
“Bahari inaunganisha nchi mbalimbali duniani na kuna mambo mengi yanafanyika katika bahari, kwa mfano uvuvi na tunajua kwamba shughuli nyingi zinazofanyika humo zinaleta athari katika mazingira,” alisema.
Alieleza mikutano ya namna hiyo huwa na mikataba ya makubaliano kwa kila nchi inayoshiriki katika utunzaji na uendelezaji wa bahari.
Alibainisha kwamba Tanzania kwa sehemu kubwa ipo karibu na Bahari ya Hindi, hivyo ni muhimu kushiriki mikutano hiyo.
“Kumekuwa na mmomonyoko wa bahari duniani, kwa hiyo dunia kwa ujumla kupitia vikao hivyo inazungumza na kupanga mikakati ya kupunguza au kuzuia changamoto zinazoikumba bahari,” alisema.
Aliongeza kwamba kilichozungumzwa na Rais Samia katika mkutano huo kuhusu kuzitaka nchi zilizoendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto za uchafuzi wa bahari ni jambo la msingi.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Dk. Tumaini Gurumo, alipongeza hatua ya Rais Samia kushiriki mkutano wa bahari nchini Ufaransa, akisema utafungua mambo mengi kwa taifa.
“Bahari ina mambo mengi ambayo yote ni maendeleo kuanzia uvuvi, utengenezaji meli, usafirishaji na hata uwepo wa madini ambapo nchi zilizoendelea zinachimba madini baharini,” alisema.
Dk. Tumaini ambaye ni mtaalamu wa sheria za bahari, alisema hii ni fursa na ndiyo maana katika ziara hiyo, rais ameonekana akitembelea katika maeneo ya utengenezaji wa vifaa na vyombo vya bahari, jambo ambalo ni jema.
“Hakika ziara hii itafungua fursa kubwa za ajira kwa kuwa hivi sasa mabaharia wa Tanzania wana soko kubwa nchi za nje, sasa ni wakati wa Watanzania kuchangamkia fursa za masomo,’’ alisema.

Alibainisha kuwa, katika ziara hiyo, Rais Samia pia aliingia makubaliano na Ufaransa kuhusu mambo mbalimbali, hivyo ni muhimu sasa jamii kuandaliwa ili kunufaika na fursa zitakazokuja.
Kwa mujibu wa Dk. Tumaini, sheria ya kimataifa ya bahari imeeleza vyema kuhusu ushirikiano na anachokifanya Rais Samia ni utekelezaji.
“Sasa tumeona mwelekeo bora kwa kuwa Tanzania bara tangu Uhuru hatujawahi kuwa na sera juu ya uchumi wa buluu, huu ndiyo wakati wake kama walivyofanya wenzetu wa Zanzibar kuwa na wizara maalumu,” alisema.
Aliipongeza serikali kwa juhudi inazozichukua katika kutekeleza uchumi wa buluu ili kuwa na tija kwa taifa, ikiwemo kuongeza ajira.
Akifafanua kuhusu mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana wa Jumuiya ya Madola kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kamati ya sera na utetezi, Delicia Mwanyika, alisema mkutano huo unalenga kuhamasisha jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kulinda uendelevu wa bahari.
Rais Samia alifanya ziara ya kwenda nchini Ufaransa na kuhudhuria mkutano huo wa siku tatu ulioandaliwa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kufanyika Februari 9 hadi 11 mwaka huu.
KANALI LUBINGA
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu, Ngemela Lubinga, akizungumzia ziara ya Rais Samia Rais Samia Ufaransa na Ubelgiji, alisema ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ili kuiwezesha serikali kupanua wigo wa uhusiano kimataifa na kuchochea fursa za uchumi.
“Hii ni fursa ndani ya CCM na taifa kwa ujumla kwa kuwa Ilani imeelekeza serikali kuimarisha uchumi na kuongeza uhusiano wa kimataifa, tumekuwa na uhusiano wa karibu na Ufaransa na Ubelgiji na nchi hizo zote zina ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania kwa kuwa wanatumia bidhaa zetu, nasi tunatumia za kwao na kufanya uwekezaji katika miradi mbalimbali,” alisema.
Kanali Lubinga alisisitiza kuwa, CCM inabariki hatua ya ziara hiyo ya Rais Samia ili kuimarisha mifumo kiuchumi na diplomasia, kwa kuwa vyama vya nchi hizo vina mengi ya kujifunza kwa chama tawala cha Tanzania ambacho ni CCM.
Aidha, aliwaondoa hofu wana CCM waliopo katika nchi hizo kuhusu uanachama wao kutokana na kutolewa kwa kadi mpya za kielektroniki, kwa kuwa mifumo inawatambua kupitia matawi yaliyopo chini ya diaspora.
“Hiki ni chama cha umma na tuna matawi nje ya nchi kupitia diaspora, hivyo wanachama wetu wasihofu, kadi mpya za elektroniki zitawafikia kwa kuwa CCM hatuna mipaka,”alisema.
MARIAM MZIWANDA Na JUMA ISSIHAKA



















