MWENYEKITI wa taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Utafiti (RAAWU), Jane Mihanji, amewahimiza waajiri na menejimenti maeneo ya kazi, kutambua dhamira njema ya vyama vya wafanyakazi katika ofisi zao.
Pia ametoa wito kwa wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na kujua kuna wajibu wakati wa kutafuta haki.
Ametoa kauli hiyo, Dar es Salaam, katika hafla fupi ya mapokezi yalioandaliwa na wanachama wa RAAWU tawi la Uhuru Publications Ltd na Peoples Media Communications Limited, ikiwa ni mara ya kwanza kuwasili katika ofisi hizo tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa RAAWU taifa.
Katika hotuba yake, mwenyekiti huyo amesema vyama vya wafanyakazi siyo wakala wa uchochezi na mivutano katika maeneo ya kazi, bali ni chombo cha kuunganisha menejimenti na wafanyakazi na kuhamasisha uwajibikaji wenye tija miongoni mwa wafanyakazi.
“Mara nyingi watu wanadhani vyama vya wafanyakazi vipo kwa ajili ya uchochezi maeneo ya kazi, wanasahau vyama hivi vipo kwa mujibu wa sheria na kusisitiza maslahi mazuri, mazingira bora ya kazi, pia vinahimiza wajibu wenye tija, kila mfanyakazi anapodai haki,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo ya kuzungumza na watumishi wa UPL na PMCL, ambayo ni matawi yaliyomlea kabla ya kushika nafasi hiyo kiuongozi, kuwataka wafanyakazi kote nchini kufanyakazi ili kuwa na nguvu ya kudai haki pale inapokosekana.
Pamoja na kuwashukuru wanachama wa RAAWU tawi la UPL, PMCL, uongozi wa kampuni hizo na wajumbe wa mkutano mkuu wa RAAWU taifa, Mihanji amesisitiza busara wakati wa kudai haki badala ya nguvu na umoja miongoni mwa wafanyakazi na menejimenti zao.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Uhuru Media Group, inayosimamia UPL na PMCL, Shaban Kisu, alisema hatua ya Mihanji kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa RAAWU Taifa, ni heshima kubwa kwa kampuni hiyo na kuahidi kushirikiana na uongozi wake ngazi ya tawi.
“Hatimaye tawi letu limetoa kiongozi wa juu taifa, kwetu hii ni heshima kubwa na tunaamini kwa utendaji wake na jinsi tunavyomfahamu hatatuangusha, RAAWU niwahakikishie mmepata mtu sahihi,” alisema.
Katika hafla hiyo, Mihanji aliambatana na Katibu Mkuu wa RAAWU Taifa, Jacob Sayo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho taifa, Simon Mbai ambao wote walichaguliwa kupitia mkutano mkuu wa RAAWU uliofanyika, Novemba 5-6, mkoani Morogoro.
Na WILLIAM SHECHAMBO



















