RAIS Samia Suluhu Hassan, amefanya mageuzi makubwa katika sekta elimu, tangu aingie madarakani kwa kuwekeza kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa sekta hiyo.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda, jijini Dar es Salam, kuhusu mafanikio katika sekta ya elimu yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia.
Profesa Mkenda amesema tangu Rais Samia aingie madarakani, ameweka msukumo mkubwa katika elimu, ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kupata elimu bora na yenye tija.
SERA
Profesa Mkenda ameeleza kwa upande wa sera ili kufanikisha hilo, wizara yake ipo katika hatua za kuifanyia marekebisho makubwa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, ambapo timu iliyoundwa inafanya kazi mkoani Morogoro, ikiongozwa na mchumi na wataalamu wa elimu.
“Rais alitoa maelekezo kwa wizara ipitie upya mitaala yote ya elimu ili kuongeza ubora na kuhakikisha kinachofundishwa kina akisi zaidi mahitaji halisi ya nchi yetu,”amesema.
Alifafanua Rais Samia anataka kuona mageuzi katika elimu na anafuatilia suala hilo kwa umakini mkubwa.
“Kazi inafanyika kuhusu mapitio ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014. Kulikuwa na kigugumizi kwamba itakuwa mzigo mzito kwenye bajeti. Wachumi tumeingia kazini kuona mzigo upo wapi? Timu inaongowa na mchumi na watalamu wa elimu. Kwa mfano sera hii inasema elimu ni lazima itakuwa siyo miaka saba bali itakuwa miaka 10.
“Sasa watu wakawa wanajiuliza kama ni miaka 10, miundombinu iko wapi. Walimu wako wapi? Uwezo wetu uko wapi?” alisema waziri huyo.
UWEKEZAJI
Profesa Mkenda alisema jambo jingine kubwa alilofanya Rais Samia ni kuongeza bajeti na uwekezaji katika elimu.
“Ukitazama fedha za Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mapambano ya Uviko – 19 katika sh. trioni 1.5. sekta ya elimu tulipata robo ya fedha hizo kwa jili ya maendeleo ya elimu, ambapo katika fedha hizo tulijenga madarasa 15,000,” alibainisha.
Mbali na hilo, alisema Rais Samia ameongoza mikopo ya elimu ya juu kutoka sh. bilioni 464 mwaka 2020/2021 hadi sh. bilioni 570 2021/2022, ameondoa tozo ya asilimia sita 6 ya thamani ya fedha katika mikopo hiyo na kuondoa tozo ya asilimia 10 kama adhabu ya kuchelewesha fedha hizo.
Profesa Mkenda alisema kuhusu elimu ya wenye mahitaji maalumu, katika mwaka mmoja wa Rais Samia, wizara imechapisha vitabu vingi zaidi, viti mwendo huku shule maalumu zikijengwa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Pia, alisema serikali imejenga vituo shikizi 3,000, ambavyo vinahudumia wanafunzi ambao wako mbali na shule jambo ambalo limeandika historia ya kipekee.
VYUO VIKUU
Profesa Mkenda alisema Rais ameandika historia ya kipekee kwa mara ya kwanza Mkoa wa Lindi utapata Chuo Kikuu ambacho kitakuwa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Tunajenga vituo vitano vya Chuo Kikuu Huri Tanzania (OUT) katika mikoa ya Geita, Simiyu, Manyara, Kigoma na Lindi na vingine tunamalizia kuvikamilisha,” alisema.
Aidha, Profesa Mkenda alisema serikali imeongeza bajeti ya kudhibiti ubora kuhakikisha inafuatilia na kusimamia ambapo sh. bilioni 5.94. zimetolewa kununua magari kwa maofisa udhibiti ubora.
Kwa upande wa sekondari, alisema sh. bilioni 17 zimetengwa kujenga shule ya sekondari ya bweni itakayochukua wanafunzi 1,000 mkoani Dodoma.
Pia, alieleza shule za sekondari 245 zitajengwa katika kata zote ambazo hazikuwa na shule hizo ambapo sh. bilioni 180 zitatumika.
Akizungumzia vyuo vya ualimu, alisemaa kuna mabadiliko makubwa yamefanyika ili kuhakikisha walimu wanaandaliwa vizuri.
“Tumejenga madarasa 41, kumbi za mihadhara tatu na mabweni 15 katika vyuo vya walimu. Pia mafunzo yametolewa kwa wakufunzi ili kuhahakikisha tunawaandaa walimu wetu vizuri,”alieleza.
MITIHANI KUSAHIHISHWA KIELEKTRONIKI
Profesa Mkenda alisema katika uongozi wa Rais Samia, uvujaji wa mitihani umepungua kutokana na udhibiti unaofanyika.
“Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limejitahidi kuwekeza. Limetengeza mfumo mzuri wa kusahihisha mitihani, unaongeza ufanisi, uhakika na kuokoa fedha,” alieleza.
Waziri alisema pia serikali inajenga vyyo vya ufundi stadi (VETA) 25 katika wilaya mbalimbali nchini na vinne mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe na Rukwa.
Kwa upande wa Vyuo vya Mendeleo ya Wananchi (FDC), alisema ukarabati wa vyuo 12 umefanyika na ununuzi wa samani katika vyuo 34 kwa thamani ya sh. bilioni 38.
Na CHRISTOPHER LISSA





























