WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda nchini, kuwapokea na kuwapa ushirikiano watu wenye ulemavu wapate fursa ya kuchangia shughuli za ujenzi wa taifa kama Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini inavyotaka.
Ameyasema hayo, baada ya kuzindua kiwanda cha kampuni ya SIKA Tanzania kinachozalisha na kusambaza kemikali zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali kilichopo Salasala. Pia Waziri Mkuu amefungua kinu namba mbili cha saruji katika kiwanda cha Twiga, baada ya kukamilika maboresho makubwa.
Akiwa katika viwanda hivyo kwa nyakati tofauti, Majaliwa alisema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha mazingira ya kufanyabiashara na hivyo kuwavutia wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Wawekezaji njooni muwekeze Tanzania, tuna ardhi ya kutosha, umeme, barabara, tuna reli ya kati na tunajenga Reli ya Kisasa, pia tuna ndege 11 na nyingine zinakuja, tunajenga viwanja vya ndege kila mkoa, hivyo tuna uhakika wa usafiri,”alisema.
Pia aliagiza Wizara ya Viwanda na Biashara iendelee na utaratibu wa kukutana na Wizara au taasisi za Serikali na binafsi nchini ili kuhamasisha kununua bidhaa zinazozalishwa nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafanyakazi wa viwanda hivyo kuwasaidia wawekezaji hao ili wakuze zaidi biashara zao na wanufaike na uwekezaji huo. “Kila mmoja asaidie ulinzi wa mali za kampuni, msikubali kushawishika kuhujumu viwanda hivi, vina manufaa kwetu.”

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo alisema ufunguzi na maboresho ya viwanda hivyo unaashiria kuboreshwa kwa mazingira ya biashara kati ya Tanzania na makampuni makubwa kama SIKA.
Kwa upande wake, Meneja Uzalishaji wa kiwanda cha SIKA, Mwijarubi Shida alisema kiwanda hicho kilianzishwa nchini mwaka 2015 na kilianza uzalishaji mwaka 2016. Alisema kiwanda kina watumishi 37 kati ya hao 36 ni wazawa.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu kabla ya kuzindua kinu namba mbili katika Kiwanda cha Saruji cha Twiga, Mhandisi Hellen Simime alisema maboresho hayo yamechangia kuongeza tani 140 katika uzalishaji wa saruji kiwandani hapo kwa mwaka. Jumla Euro milioni 3.5 sawa na shilingi bilioni tisa zimetumika katika maboresho hayo.
NA MWANDISHI MAALUMU





























