JESHI la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani limepiga marufuku kwa pikipiki, maarufu kwa jina la bodaboda, kubeba wanafunzi wenye umri wa kuanzia miaka mitatu hadi saba na kusema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya dereva atakayekiuka agizo hilo.
Pia, jeshi hilo limeanzisha operesheni maalumu kwa magari na bajaji yanayobeba watoto wa shule kinyume na uwezo wa vyombo hivyo vya usafiri.
Aidha, jeshi hilo limefanikiwa kulikamata gari dogo aina ya Toyota hiace, ambalo lilibeba wanafunzi 49 na msimamizi wa Shule ya Msingi Magufuli, iliyopo Mbeya mjini na msimamizi wao, huku gari hilo likiwa halina usajili wa kubeba wanafunzi.
Akizungumza na UhuruOnline, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa, amesema operesheni hiyo iliyoanza Septemba 18, mwaka huu, kukagua magari madogo na mkubwa imesadia kukamatwa kwa gari hilo.
Mutafungwa alisema gari hilo lilivunja sheria kwa kubeba wanafunzi wengi, huku likiwa halina kibali.
Hata hivyo, Kamanda Mtafugwa amesema dereva na msimamizi wa watoto hao, walikamatwa alfajiri na uchunguzi unaendelea kwa mmiliki wa gari hilo, kwa kulitumia gari hilo kinyume na leseni aliyolisajilia.
“Vitendo vya upakiaji wanafunzi kinyume na uwezo wa gari vinakatazwa na wanatakiwa kusafirishwa katika magari yaliyosajiliwa, kwa idadi sahihi kulingana na uwezo wa gari,” alisema.
Aidha, Kamanda Mutafungwa alibainisha kuwa wamiliki wa magari wanatakiwa kufuate kanuni na sheria za kuwabeba wanafunzi katika hali ya usalama.
Vile vile, aliwataka wakuu wa shule kutokwepa majukumu yao na wawe makini kufuatilia magari yanayobeba wanafunzi hao.
“Wazazi wana jukumu la kuwa waangalifu kufutilia usafiri wanaopanda watoto wao na akiona dosari ya aina yoyote, ikiwemo kujaa kwa gari hilo watoe taarifa sehemu husika,”alisema.
PIKIPIKI, BAJAJI
Akizungumzia usafiri wa pikipiki na bajaji alisema kwa upande wa bajaji wanaruhusiwa abiria watatu tu na pikipiki haruhusiwi kupanda mwanafunzi mdogo, kwa kuwa hana uwezo wa kuvaa kofia ngumu.
Kamanda Mutafungwa alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi watakapoona matukio kama hayo.
Pia, jeshi la polisi linafanya uchunguzi kwa madereva wanaotumia pombe wakati wa kuendesha magari ya shule.
“Nawapongeza askari wote mkoani Mbeya kuendesha operesheni kwa umakini na kufanikiwa kulikamata gari lililobeba wanafunzi wengi,” alisema.
WADAU WATOA MAONI
Saidi Michuzi, mwendesha bodaboda anayeegesha pikipiki yake Mtaa wa Livingstone na Uhuru, alisema kinachowashawishi baadhi ya wazazi kutumia usafiri wa huo kuwapeleka na kuwarudisha watoto wao shuleni, ni unafuu kwa maana ya nauli.
“Mimi kama bodaboda akija mteja siwezi kukataa kwa kuwa najua hiyo ni kazi ya uhakika ambayo itaniingizia kipato. Hata hivyo napaswa kuzingatia usalama wa mtoto kwa kuhakikisha nambeba katika mazingira salama na kutoendesha kwa mwendo wa kasi,” alisema.
Kwa upande wake Zainab Selemani, mkazi wa Mjimwema, Kigamboni Dar es Salaam, alisema ingawa kusafirisha watoto kwa pikipiki kwenda na kurudi shuleni ni rahisi, lakini mzazi au mlezi anapaswa kukumbuka na hatari zinazoweza kumpata mtoto husika.
“Tusitazame urahisi tu, bali tuangalie na madhara, lakini na polisi nao watusaidie wazazi kuhakikisha sheria za barabarani zinazingatiwa ili watoto wetu waendelee kuwa salama,” alisema.
Hamisi Mohammed mkazi wa Vingunguti, Dar es Salaam alisema kuwa mabasi ya shule yamekuwa na gharama kubwa, ambapo hutakiwa kulipa sh. 300,000 kwa muhula ilhali bodaboda kwa mwezi analipa sh. 30,000 tu.
REHEMA MAIGALA na ASHURA ASSAD





























