RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais Yower Museveni wa Uganda, wametangaza neema na fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara kwa wananchi wa pande hizo mbili na ukanda mzima wa Afrika Mashariki, kwa kuondoa vikwazo mbalimbali.
Kutokana na kuondolewa kwa vikwazo hivyo vya kibiashara, sasa wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili wanaweza kufanya biashara yenye tija katika nchi hizo mbili.
Hayo, yamejitokeza katika ziara ya kikazi ya Rais Samia nchini Uganda, ambapo alisema hatua hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa Tanzania na Uganda zinaushirikiano wa kindugu wa muda mrefu.
MAKUBALIANO
Baada ya mazungumzo yao, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Uganda katika mkutano huo ilisema, Marais hao wamekubaliana kujengwa na kuimarishwa kwa soko la Mutukula, ambalo litakuza biashara baina ya nchi hizo na kuwanufaisha wananchi wa pande zote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu ya Uganda, kuwa uimara wa soko la Mutukula sio tu utawanufaisha wananchi wa Uganda na Tanzania, bali ukanda wote wa Afrika Mashariki na kustawisha maisha yao.
Viongozi hao pia walishuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ya maendeleo; ukiwemo wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Uganda kuja Mwanza Tanzania, kupitia MutukulA-Kyaka-Nyakanazi-Mwanza. Pia walishuhudia mkataba wa kuimarisha ulinzi.
Viongozi hao pia walieleza kuhusu hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.
Mbali na hayo, viongozi hao walielekeza kutekelezwa kwa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha pande mbili hizo kilichofanyika Januari mwaka huu.
Kuhusu uchumi, taarifa hiyo ilieleza pia Rais Samia na Rais Museveni walikubaliana kuimarisha sekta hiyo, ikiwemo kuridhia ushirikiano katika biashara ya dawa ambapo Tanzania itanunua kutoka Uganda.
Aidha, ilieleza kuwa kwa ajili ya kulilinda bomba la mafuta ghafi, kuanzia mwaka ujao wa fedha unaoanzia Julai mwaka huu, Tanzania itaanza kutoza dola 10 kwa kila kilomita 100 kwa kila lori kutoka Mutukula hadi Dar es Salaam.
“Uganda itasambaza tani 10 za sukari nchini Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na upungufu uliopo. Pia, wamekubaliana kuendelea kuisaidia sekta binafsi kwa ajili ya kuimarisha ukuaji uchumi, ambapo Rais Samia atafanya mazungumzo na sekta binafsi, ikiwemo kukutana na viongozi wa sekta hiyo wa Uganda,” ilisema taarifa ya makubaliano yaliyofikiwa na viongozi hao.
Ilisema Rais Samia na Rais Museveni walitazama ukuaji wa biashara baina ya nchi mbili hizo na kuwaagiza mawaziri wanaosimamia sekta hiyo kutoka pande zote mbili kuondoa vikwazo, ili kuharakisha biashara baina ya nchi hizo.
Pia, katika ziara hiyo ya siku mbili ya Rais Samia nchini Uganda, nchi hizo zimekubaliana mambo mbalimbali, likiwemo la ufanyaji wa biashara pamoja baina ya nchi hizo kupitia Bandari ya Mwanza hadi Port Bell nchini Uganda, ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) itasafirisha mizigo ya wafanyabiashara.
Pia, makubaliano mengine waliyoyafikia ni kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na uchumi, pamoja na kushirikiana katika ujenzi wa miundombinu ya kimaendeleo katika maeneo ya nishati ya maji, mafuta na usafiri wa barabara.
Aidha, Rais Samia na Museveni pia waliingia makubaliano katika masuala ya afya, likiwemo la kuanzisha kiwanda cha dawa za mifugo na chanjo ili kuwaisadia wananchi wa maeneo hayo na kuzalisha ajira za moja kwa moja 3,000 hadi 10,000.
Mazungumzo hayo ya Marais, pia yalifikia makubaliano juu ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda, ambapo leo Rais Samia anatarajia kuzungumza na wafanyabiashara mbalimbali katika sehemu ya kuhakikisha wanaondoa vikwazo na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.
RAIS SAMIA
Akizungumzia ziara hiyo, Rais samia, alisema wemekubaliana na Rais Museveni kuanzia sasa mawaziri wa kisekta wa nchi hizo mbili watakutana mara kwa mara, kwa ajili ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa nchi hizo.
Kuhusu mapokezi, Rais Samia alishukuru kwa kupata mapokezi mazuri akiwa na msafara wake, hivyo anajisikia yuko nyumbani kwa kuwa Tanzania na Uganda zina ushirikiano wa kindugu na wa muda mrefu ukiwa wa kihistoria.
Alisema ni mara ya kwanza kwenda Uganda kwa mwaliko rasmi wa kikazi, lakini amebaini kuwa Uganda na Tanzania ni nchi zenye ushirikiano wa kutosha wenye historia ya kipekee.
“Nimepata mapokezi mazuri mimi binafsi na msafara wangu wote. Najisikia niko nyumbani. Tanzania na Uganda pamoja na nchi zingine zinapitia wakati mgumu ikiwemo ugonjwa wa Uviko-19 na pamoja na vita inayoendelea sasa kati ya Ukraine na Russia’’ alisema.
Rais Samia alisema ni wakati sahihi wa kuwa pamoja na kuchukua hatua za kupambana na uchumi wa nchi hizo, ambapo amekuja Uganda kwa ajili ya kuangalia njia bora ya kudumisha ushirikiano uliopo na kutangaza fursa za kibiashara nchini Tanzania.
Alisema katika kikao cha ndani, wamezungumza mambo mbalimbali yanayokwenda kudumisha ushirikiano na kuingia makubaliano yenye kuimarisha umoja na ushirikiano, biashara, ulinzi na usalama baina ya nchi hizo mbili ili kukuza ushirikiano wa kihistoria uliopo.
‘’Nawaomba sana wafanyabiashara na wawekezaji wa Uganda kuja Tanzania kwa kuwa ni mahala salama na kuna kila aina ya uwekezaji mnaoutaka. Nimejifunza na kuona namna ya ujenzi bora wa uchumi unaofanywa na Rais Museveni licha ya kupitia changamoto mbalimbali, ikiwemo ya Uviko-19 bado anatekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi’’ alisema.
RAIS MUSEVENI
Kwa upande wake, Rais Museveni alisema anamshukuru Rais Samia kwa ziara hiyo huku akimuahidi yote waliyokubaliana atayasimamia ili maisha ya wananchi wa nchi zote mbili wanufaike na ushirikiano uliopo wa Uganda na Tanzania.
Rais Museveni, alisema kitu kilichowaweka pamoja ni kwa maslahi ya nchi hizo ni kufanyia kazi ushirikiano uliopo katika masuala ya usalama, miundombinu, uchumi na biashara.
NA MWANDISHI WETU





























