SERIKALI imetenga sh. bilioni 37.85 kujenga nyumba za walimu katika shule za sekondari na sh. bilioni 43.63 kwa shule za msingi.
Kauli hiyo ilitolewa Bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Segerea (CCM), Bonnah Kamoli.
Mbunge huyo alitaka kujua lini serikali itatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo kwa kuhakikisha inajenga nyumba za walimu kama inavyofanya kwa majeshi ya ulinzi.
Akijibu swali hilo, Silinde alisema serikali inatambua changamoto ya mahitaji ya nyumba za walimu nchini.
Alisema ili kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo, serikali itaendelea kupeleka fedha za kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu kulingana na upatikanaji wa fedha kupitia vyanzo mbalimbali.
“Katika mwaka wa fedha 2022/2023, serikali imetenga shilingi bilioni 37.85 za ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za sekondari na shilingi bilioni 43.63 za ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za msingi,” alieleza.
Naibu waziri huyo alisisitiza serikali itaendelea kutoa fedha za nyumba za walimu katika maeneo ambayo kunauhitaji mkubwa likiwemo na Jimbo la Segerea kadri fedha zitakavyopatikana.
NA MUSSA YUSUPH



























